Jumanne, 24 Machi 2015

MAGAZETINI LEO

AFANDE SELE KUINGIA KWENYE ULINGO WA SIASA KUPITIA ACT.

MWANAMUZIKI wa kizazi kipya, Suleimani Msindi ‘Afande sele’, ametangaza nia ya kuwania ubunge wa Morogoro mjini kupitia Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Tanzania). Msanii huyo ametangaza azma yake hiyo jana mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, baada ya kujiunga na chama hicho akitokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). “Niliumizwa baada ya kusikia kuwa eti katiba ya chama inasema kuwa mwanachama anayekwenda mahakamani kudai haki yake anakuwa amejivua uanachama wake. Kwa chama kama Chadema sikuamini kama kingekuwa na sheria kandamizi kama hiyo ya kuzuia wanachama wake kwenda mahakamani, ambacho ndicho chombo cha mwisho kwa mtu kudai haki,” alisema. Akielezea sababu nyingine iliyomfanya kujitoa Chadema imechangiwa na kuondolewa kwa Zitto Kabwe, ambaye alichangia kumhamasisha kujiunga na chama hicho. “Jambo jingine nililojiuliza ni kwamba kama mti mbichi (Zitto), umetendwa hivyo je, mimi mkavu itakuwaje nikaona bora nivue ukamanda nivae utaifa kwanza,” alisema Afande Sele.

MKAPA ATETEA UWEKEZAJI

Rais mstaafu Benjamin Mkapa amesema sekta ya uwekezaji nchini inashindwa kukua kwa kasi inayotarajiwa kutokana na baadhi ya wanasiasa kutokuielewa vizuri. Akizungumza leo wakati wa kusaini makubaliano ya kusaidia kuvutia na kuongea uwekezaji wa ndani na nje nchini kati ya Taasisi inayoshughulikia mazingira ya uwekezaji Barani Afrika (ICF) na Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Mkapa ambaye pia ni Mwenyekiti mwenza wa ICF alisema baadhi ya watu wanautazama uwekezaji kama unyonyaji. “Watu wanaona wanataka kunyonywa na sio kunyonyana,” alisema Mkapa wakati akielezea mafanikio ya TIC tangu kuanzishwa kwake. Chini ya makubaliano hayo yaliyosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa ICF, William Asiko na Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Juliet Kairuki, ICF itakisaidia kituo cha uwekezaji nchini kukuza, kuinua na kulingaza dirisha la uwekezaji na kuimarisha uwezo wake katika kuwezesha na kufuatilia uwekezaji nchini. Kairuku alisema Dola 950,000 (Sh1.7 bilioni) zitatolewa kwa ajili ya mradi wa dirisha la uwekezaji Tanzania ambazo zitachangwa kwa pamoja kati ya ICF na Serikali ya Tanzania kwa lengo la kurahisisha huduma zote zinazotolewa TIC kupatikana haraka, kwa ufanisi na bila kupoteza muda. “Huduma zote zinazotolewa na TIC sasa zitakuwa zikipatikana mtandaoni ikiwa ni pamoja na kulipia ada mbalimbali, tunajaribu kuwa wa kisasa,” alisema Kairuki na kuongeza kuwa huduma hiyo itawanufaisha zaidi wawekezaji wa mikoani. Mpango huo unatarajiwa kuwapa wananchi nafasi ya kupata huduma zote za kituo hicho kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Idara ya Uhamiaji, Wizara ya Ardhi, Mamlaka ya HIfadhi za Jamii (SSRA) na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) kwa kutumia mfumo wa kieletroniki. Mwenyekiti mwenza wa ICF, Neville Isdell alisema uwekezaji unahitaji uwazi ili kuwavutia wafanyabiashara wa ndani na nje kuendelea kuwekeza. “Biashara zote hususani zilizo ndogo zinahitaji kuwa na mazingira yaliyo mazuri watakayofanyia shughuli zao. Kwa kuwa na dirisha la uwekezaji biashara nyingi zitaweza kukua, kuongezeka na kushamiri haraka,” alisema Isdell. Waziri wa Uwekezaji na Uwezeshaji, Christopher Chiza alisema mradi huo utakapokamilika utasaidia kuboresha mazingira ya biashara na ushindani nchini. “Kwa muda wa miaka michache iliyopita nafasi ya Tanzania kimataifa katika kufanya biashara kwa mujibu wa ripoti mbalimbali imekuwa hairidhirishi, ishara ambayo sio nzuri kwa wawekezaji na sekta binafsi,” alisema Chiza.

JK POLISI KUWENI TAYARI

Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amelikata Jeshi la Polisi nchini kujiandaa kikamilifu ili kukabiliana na vurugu zozote zitakazojitokeza wakati wa uandikishaji wapigakura, upigaji Kura ya Maoni ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu. Akifunga mafunzo ya maofisa warakibu wasaidizi katika Chuo cha Taaluma ya Polisi, Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema dalili zinaonyesha kwamba kuna watu wenye nia ya kuhatarisha amani katika matukio hayo. “Tunayoyasikia na tunayoyaona yanaashiria kuwapo kwa dalili za wenzetu kukwamisha shughuli hizi za kitaifa kwa kufanya vurugu, Jeshi la Polisi jiandaeni na vitendo vyote vitakavyofanywa kwa lengo la kuhatarisha amani,” alisema akijibu maombi ya kupatiwa vifaa yaliyowasilishwa kwake na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu. Alisema Serikali itahakikisha kazi ya uandikishaji katika daftari la wapigakura, upigaji wa kura ya maoni na uchaguzi mkuu vinafanyika kwa amani na utulivu kwa gharama zozote. Alisema ili kufanikisha kazi hiyo, Serikali italiwezesha Jeshi la Polisi ili litekeleze kikamilifu majukumu yake ya kulinda amani na utulivu. “Tutawawezesha kwa kuwapa vifaa ili kuhakikisha mnafanya kazi yenu ya kutunza amani kwa umakini zaidi,” alisema Rais Kikwete anayemaliza muda wake wa mihula miwili ya urais baada ya uchaguzi mwaka huu. Iwapo mambo yote yatakwenda kama yalivyopangwa, Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa itapigwa Aprili 30 wakati Uchaguzi Mkuu utafanyika Oktoba. Profesa Lipumba apinga Akizungumzia kauli hiyo ya Rais Kikwete, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema, “Rais Kikwete yeye ndiye mtu wa kwanza kuivuruga amani kwa kutangaza tarehe ya kufanyika kwa kura ya maoni wakati siyo jukumu lake na jukumu hilo ni la NEC, Serikali yake kushindwa kuratibu vyema mchakato wa uandikishaji. “Kama uandikishaji hauendi vizuri mpaka sasa, anavunja sheria za nchi halafu yeye mwenyewe tena anakwenda kwa vyombo vya dola na kuvieleza vijiandae wakati yeye huyohuyo ndiye ameanzisha uvunjifu wa amani tunashindwa tumweleweje,” alisema. Profesa Lipumba alisema kinachotakiwa kufanyika kwa sasa ni NEC kutangaza tarehe kamili ya uchaguzi na uandikishaji uende kwa utaratibu tofauti na ilivyo sasa kwa mkoa mmoja wa Njombe kusuasua mambo ambayo yanaashiria uvunjifu wa amani.

Ijumaa, 20 Machi 2015

KUELEKEA EL CLASSICO

Kuelekea EL CLASSICO Messi akiwa katika kiwango cha juu kabisa huku Christiano Ronaldo na real madrid wakilalamikiwa na mashabiki zao kutokuonesha kiwango kikubwa tutegemee nini kuktoka kwa Lionel Messi aliye onesha kiwango cha juu katika mechi ya klabu bingwa ulaya (UEFA) dhidi ya Man City.

MKAPA NA UTEUZI WA VIONGOZI

RAIS mstaafu, Benjamin Mkapa, amekosoa uteuzi wa viongozi wa umma nchini akisema sera ya utumishi wa umma inayojali utaalamu haifuatwi. Ametoa kauli hiyo wiki chache baada ya kuzuka mjadala wa uteuzi wa wakuu wa wilaya uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete, huku ikielezwa haukuzingatia weledi, maadili na uzoefu kwa walioteuliwa. Akizungumza katika siku ya pili ya uzinduzi wa Kavazi la Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam jana, Mkapa aliyekuwa mtoa mada, alisema kutojali taaluma ni kati ya mambo yanayorudisha nyuma maendeleo ya nchi. “Jambo moja ninalodhani limeturudisha nyuma katika maendeleo na mnisamehe kwa kusema hili, ni sera ya utumishi wa umma. “Tunajua kanuni za kuhamisha mtu kutoka sehemu moja kwenda nyingine, iwe ni kwa utawala wa jumla au kwenye nafasi za utaalamu. Hapa ndipo tulipopotea. “Mzee Msuya (Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya) atakuwa amewaambia, wakati ule hata ukimaliza chuo kikuu, bado utapewa nafasi kama ofisa maendeleo ya jamii na utapitia mafunzo ili kupanda vyeo. “Utakuwa ofisa mwandamizi au hata kamishna, lakini leo unaweza ukawa mtu yeyote na ukapangwa popote,” alisema Mkapa huku akishangiliwa na washiriki wa kongamano hilo. Akijibu swali kama nchi za Afrika zinaweza kuendelea huku zikitegemea misaada ya wahisani, Mkapa alisema nchi zilizoendelea zina mkakati wa kuhakikisha nchi zinazoendelea haziendelei. “Ni kweli, tunaambiwa kwamba tunashindwa kushindana na uchumi wa nchi zilizoendelea na hii ni kwa sababu wana mkakati wa kuhakikisha hatuwafikii, wanataka unyonyaji wao uendelee,” alisema Mkapa. Akizungumzia umasikini unaolikabili Bara la Afrika, alisema jukumu la Serikali ni kuwajibika katika kuondoa umasikini wa kipato, chakula, elimu, afya, watu kushindwa kumiliki mali na kutoshiriki katika siasa. Alisema kuwajibika kwa Serikali ni muhimu katika kujenga mfumo wa uchumi na umilikaji wa rasilimali kwa wananchi. “Kwa sababu wananchi wengi ni wakulima wadogo na wafugaji, kigezo kikubwa cha maendeleo ni kuwamilikisha ardhi,” alisisitiza Mkapa. Kuhusu dira ya taifa, alisema Serikali inatakiwa kuitofautisha na mipango ya maendeleo ya kila mara ili ieleweke. Awali, akitoa mada ya kurejea kwa maendeleo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Uchumi na Mipango ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa na Afrika, Profesa Adebayo Olukoshi, alisema jukumu la Serikali duniani kote ni kupambana na umasikini wa wananchi wake.

AJALI MJINI MBEYA

Abiria wapatao 65 wamenusurika kifo baada ya Basi la Nganga Express linalo fanya safari yake Mbeya - Dar, kuingia mtaroni katika harakati za dereva kukwepa Lori lililokua likija uso kwa uso uso kwa uso.kitendo hicho kilikoa roho za abiria na wafanyakazi wa Basi hilo. Majeruhi wa5 wamekimbizwa hospitali ya rufaa Mbeya. Ajali hii imetokea Mbeya kijiji cha Lilongo asubuhi hii majira ya 12.48.

Alhamisi, 19 Machi 2015

TWIGA STARS KUTUA ZAMBIA KESHO

Timu ya Taifa ya Tanzania ya Wanawake (Twiga Stars), inatarajiwa kuondoka nchini siku ya ijumaa kuelekea nchini Zambia kwa ajili ya mchezo wake wa kwanza dhidi ya timu ya Taifa ya Wanawake ya Zambia siku ya jumapili. Twiga Stars inaanzia hatua ya pili katika kuwania kufuzu kwa Fainali za Afrika kwa Wanawake baada ya kuwa katika nafasi za juu kwa viwango barani Afrika, na endapo itafanikiwa kuwaondoa Wazambia itafuzu moja kwa moja kwa fainali hizo. Msafara utaongozwa na Blassy Kiondo (Mjumbe wa Kamati ya Utendaji), Beatrice Mgaya (kiongozi msaidizi), Rogasin Kaijage (kocha mkuu), Nasra Juma (kocha msaidizi), Furaha Francis (Meneja), Christine Luambano (Daktari) na Mwanahamis Abdallah (Mtunza vifaa). Wachezaji watakokweda Zambia ni Asha Rashid, Mwajuma Abdallah, Mwanahamis Omar, Donisi Minja, Amina Bilal, Fatuma Bashiri, Esther Chabruma, Shelda Mafuru, Maimuna Kaimu, Najiat Abbas, Stumai Abdalla, Fauma Issa, Thereza Yona, Fatuma Hassan, Fatuma Omary, Sophia Mwasikili, Fatuma Khatibu na Etoe Mlenzi.

KANISA LILILOPITISHA NDOA ZA JINSIA MOJA

Kanisa la Presbyterian nchini Marekani ambalo lina takriban wanachama millioni 2 ,limebadilisha sheria yake ya ndoa na kuwajumuisha watu wa jinsia moja. Kanisa hilo ambalo linashirikisha idadi kubwa ya wanachama wake duniani lilitoa tangazo hilo baada ya idadi kubwa ya magavana wa majimbo yake 171 kuidhinisha mabadiliko hayo. Sheria yake mpya sasa itasoma kwamba ndoa ni makubaliano ya kipekee kati ya watu wawili ikilinganishwa na makubaliano kati ya mume na mke. Sheria hiyo ilioidhinishwa na baraza kuu la kanisa hilo mwaka uliopita ilikubaliwa na zaidi ya nusu ya majimbo ya kanisa hilo. Mkutano wa makundi katika jimbo la New Jersy ulikuwa wa 86 kuidhinisha sheria hiyo. Uamuzi huo unatarajiwa kuzua mgawanyiko mkubwa kati ya wanachama wa kanisa hilo ambao wanapinga sheria hiyo. Mwaka uliopita baraza kuu la kanisa hilo lilitoa idhini kwa wachungaji wake kuwafungisha ndoa wapenzi wa jinsia moja katika majimbo ambayo ndoa hizo zinaruhusiwa. BBC swahili

MUSWADA WA SHERIA YA KURATIBU AJIRA ZA WAGENI WAPITISHWA BUNGENI

DODOMA. WAZIRI wa Kazi na Ajira Mhe. Gaudensia Kabaka amesoma Muswada wa Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni nchini wa mwaka 2014 kwa mara ya pili ikiwa muswada huu umelenga masuala mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya kiuchumi pamoja na mahitaji ya kiteknolojia ambayo ni kichocheo kikubwa cha uhamiaji wa nguvu kazi kutoka nchi moja kwenda nyingine. Mhe.Kabaka alisema kwa sasa zipo mamlaka nyingi zinzotoa vibali vya ajira kwa wageni kwa kuzingatia sheria zinazosimamia maswala ya Uhamiaji, Uwekezaji, Elimu, Biashara na Wakimbizi, hivyo hali hii ya kuwepo na mamlaka nyingi zinachangia kusababisha usumbufu kwa wawekezaji na kokosekana kwa uwajibikaji pamoja na kuwepo na udanganyifu. “Kutungwa kwa sheria hii kunalenga kutelekeza kwa manufaa ya nchi yetu mikataba ya kikanda inayoruhusu uhamiaji huru wa nguvu kazi hususani inayohusu itifaki ya soko la pamoja la Jumuiya ya Afika Mashariki na Ushirikiano wa Jumuiya ya nchi za kusini mwa Afrika SADC” alisema Mhe. Kabaka. Katika kutekeleza mikataba ya kikanda na kimataifa kuhusu uhamiaji na nguvu kazi, utaratibu wa kutoa vibali vya ajira kwa wageni umekuwa ukitumika ili kuhakikisha nguvu kazi ya wageni hao inaleta manufaa kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na pia katika kulinda ajira za wananchi. Kwa upande wa Msemaji Mkuu wa kambi rasmi ya upinzani Mhe.Celina Paresso Mbuge wa Viti Maalum-CHADEMA aliishauri Wizara ya Kazi na Ajira kushirikiana na wizara mtambuka kama Wizara ya Viwanda na Biashara na Idara ya Uhamiaji, kufanya ukaguzi wa vibali vya ajira hasa katika maeneo ambayo raia wa kigeni wanafanya shughuri zao bila kuzingatia sheria za nchi. “Tanzania tuna maliasili nyingi, lakini dunia ya leo na ijayo itatawaliwa na wenye maarifa, kwa maana ya sayansi, teknolojia, elimu na ujuzi” alisema Mhe. Paresso “kuwa na maliasili peke yake haitoshi, hatuna
budi tujinoe kwa elimu na ujuzi, na hasa elimu inayomuwezesha mtu aajirike au ajiajiri” aliongezea Mhe. Paresso Endapo Mhe. Rais ataridhia, Sheria hii itaanza kutumika tarehe 1 Julai, 2015. Kutungwa na kuanza kutumika kwa Sheria ya Ajira ya Wageni Nchini kutakuwa na matokea chanya ikiwema uratibu mzuri wa ajira za wageni nchini, kuongezeka kwa ajira za watanzania na kuongezeka kwa ujuzi kwa wafanyakazi wa Tanzania. Credit to Tanzania today.