Jumatatu, 25 Agosti 2014
BARA LA PILI LA UCHINA
Bara la Pili la Uchina:
Namna gani mamilioni ya wahamiaji kutoka China yanavyojenga himaya Afrika
Howard W. French
Tunawaona Wachina kila mahala katika jiji la Dar es Salaam na viunga vyake. Tunakula kwenye migahawa ya Kichina. Barabara zetu nyingi zinajengwa na kampuni za Kichina. Madaraja na majengo mengi marefu jijini Dar es Salaam yanajengwa na kampuni za kichina. Tunavaa nguo kutoka China. Vyama vya siasa vinaagiza vifaa vyao vya uhamasishaji kutoka China. Ni China ni China ni China. China imeteka bara la Afrika na Tanzania. Ni kwa namna gani Uchina imetawala Afrika kupitia kwa raia wake utapata baada ya kusoma kitabu hiki. Wachina wanakuwa walowezi katika bara la Afrika na kuendesha biashara, kilimo na viwanda.
Mwandishi Howard French anasimulia safari zake za bara zima la Afrika kukutana na walowezi wa kichina na kuzungumza nao kuhusu sababu zilizowapelekea kuhamia Afrika. Simulizi hizi zimezaa kitabu cha kurasa 285 kilichotoka mwaka 2014 na kupigwa chapa na Alfred A. Knopf. Nilikutana na mwandishi huyu jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa mwezi huu. Ingawa kitabu chake nilikipata mwezi Julai kutoka kwa rafiki yangu nchini Zambia, sikuwa nimekisoma nilipokutana na mwandishi. Nimekimaliza na ninakipendekeza kwa wasomaji wangu wa safu hii. Mwandishi French ameandika kitabu kingine kiitwacho ‘Bara la kujichukulia’, ameonyesha umahiri wake katika kusimulia ujio wa walowezi wa Kichina barani Afrika.
Safari yake inaanzia Msumbiji kwa mkulima wa Kichina, kwenda Zambia kwa tajiri wa madini ya shaba na Senegal kwa mchuuzi na mjenzi wa majumba. French amepita Dar es Salaam na kukutana na machinga wa kichina, Liberia kwa wakata magogo, Ghana kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu na Guinea na Sierra Leone kwa miradi mikubwa ya uchimbaji madini. Kote Bwana French anaeleza namna ambavyo raia wa kichina wamemiminika na kufanya kila aina ya shughuli ambazo hazikuwahi kufikiriwa kufanywa na wageni. Wachina wengi wanaokuja kwenye miradi mbalimbali, kwa mfano, kandarasi za barabara huishia kubakia kwenye nchi husika na kuanza kuamua kuishi.
French anaelezea simulizi zake na walowezi hawa ambao wanajenga miundombinu ya barabara, reli na bandari mpaka wanaofanya biashara ya ukahaba katika miji kama Maputo na Dakar. Hadithi kubwa wanayotoa, licha ya wengine kuonekana kabisa wakidharau watu weusi, ni kwamba Afrika inawapa fursa nzuri kuliko nchi yao. Kwamba wana uhuru zaidi wa kufanya mambo yao na pia wanapata faida kubwa zaidi. Hata hivyo inaonyesha kuwa Serikali ya China inashawishi raia wake kulowea Afrika. Katika moja ya simulizi hizi, aliyekuwa Waziri wa Fedha wa Zambia ananukuliwa akirejea raia walizokuwa wanapewa na viongozi wa Serikali ya China kwamba ‘Afrika ilegeze masharti ya kiuhamiaji kwa raia wao’.
Mahusiano ya kibiashara kati ya Uchina na Afrika yamekuwa yakiongezeka kwa kasi sana katika muongo mmoja uliopita. Biashara kati ya China na Afrika ilikua kufikia thamani ya dola za kimarekani bilioni 200 mwaka 2012, mara ishirini zaidi toka milenia mpya. Mabenki, makampuni ya ujenzi na makampuni mengine yamezagaa bara zima la Afrika kutafuta fursa ya kufanya biashara, kununua malighafi na kupata masoko ya biadhaa zao ambazo ni nafuu kuliko kutoka nchi za Ulaya na Marekani.
Kisera, Uchina imekuwa ikichukua mtindo wa bidhaa kwa bidhaa ‘barter trade’ katika mtindo wa kisasa inapofanya biashara na Afrika. Mwandishi ameeleza kwa ufasaha sana namna ambavyo nchi kadhaa za kiafrika zinavyolipia miradi kutoka China kwa kutumia rasilimali zake za madini na mafuta na gesi. Mfano mzuri ni wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambayo ilitoa ruhusa kwa China kuchuma utajiri wake wa madini ya shaba na bati huku yenyewe ikijengewa barabara, hospitali na mashule. Mradi huu ulikuja kuonekana umegubikwa na rushwa za kila namna.
China pia hutoa fedha zake kwa miradi ambayo inaendeshwa na makampuni kutoka China, mali ghafi kutoka China na hata wafanya kazi kutoka China. Hapa Tanzania kuna mradi mkubwa wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam wenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 1.3. Mkopo wa wa kujenga mradi huu umetolewa na Benki ya Exim ya China lakini Tanzania haitaona hata shilingi moja sababu makampuni yote ya ujenzi yanatoka China, malighafi za ujenzi zinatoka China na hata wafanyakazi wa chini kabisa ni wafungwa kutoka magereza ya China. Wizara ya Fedha ya Tanzania inafanya kazi ya kurekodi tu matumizi ili iweze kulipa deni hilo litakapoiva. Wachina wanaojenga bomba wengi watabakia nchini na wengine tayari wanatuhumiwa kuhusika na ujangili wa pembe za ndovu.
Katika kitabu hiki utakutana na simulizi za kuchukiza namna ambavyo viongozi wa Afrika wanavyohusika na rushwa ili kusaidia makampuni ya Kichina kupata biashara au kupata haki za kunyonya rasilimali madini. Utaona mahusiano kati ya viongozi wa Serikali ya Angola na makampuni ya mafuta ya Uchina na jinsi mradi wa kujenga nyumba za kupangisha juu ya uwanja wa mpira ulivyoleta malalamiko nchini Senegal kiasi cha Rais mpya wa nchi hiyo kuufutilia mbali. Awali Rais aliyetangulia Abdilahi Wade alihusishwa na rushwa ya kutoa kibali cha ujenzi huo.
Nchini Guinea Conakry kulikuwa na Mtawala Dadis Camara ambaye alichukua nchi baada ya kumpindua Lansana Conte. Mwanajeshi huyu aliingia mikataba ya haraka haraka na kampuni ya Kichina ya kunyonya utajiri wa madini ya chuma na Bati ilia pate majenereta ya kuzalisha umeme katika jiji la Conakry. Umeme huo ulikuwa muhimu kwa uchaguzi kwani hakuna Rais nchini humo aliyeweza kufanya hivyo toka uhuru mwaka 1958. Dili hilo liliota mbawa na mtawala huyo aliondolewa madarakani na wenzake. Huu ni mmoja wa mifano mingi utaikuta kwenye kitabu hiki.
Ni namna gani Afrika imejipanga kuhusu changamoto hii ya walowezi wa kichina? Ni uamuzi wa Waafrika wenyewe, ama kuwa koloni kwa mara nyingine au kutumia fura hii kujenga mahusiano yatakayoondoa ufukara uliotapakaa kwa wananchi wa Afrika. Naona Wazungu nao sasa wanaanza kuwaonea wivu Wachina. Tunanyonywa na Mzungu au Mchina, au tutakataa kunyonywa na yeyote?
BY ZITTO KABWE
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni